Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Muhammad Amrū, msimamizi wa eneo la Jabal Lebanon na Kaskazini, katika hafla ya kumbukumbu iliyoandaliwa na Hizbullah pamoja na familia ya shahidi Issa Abdullah Amrū, aliyepata shahada katika mapambano ya “Ūlī al-Ba’s” huku akiitetea Lebanon na wananchi wake, alisisitiza kuwa mashinikizo ya kisiasa dhidi ya Lebanon hayatatoa matokeo yoyote ilimradi mshikamano wa kitaifa unabaki kuwa nguzo kuu na ngome ya nchi.
Katika hafla hiyo, iliyohudhuriwa na kundi la wanazuoni wa dini, wanaharakati wa kijamii, wajumbe wa halmashauri za miji, wakazi wa eneo husika na familia za mashahidi, alibainisha kuwa kuondoa au kupuuza nguzo moja ya msingi ya Lebanon ni ndoto na mawazo yasiyo na uhalisia.
Mwanachama huyo wa Hizbullah alieleza kuwa; Muqawama unataka Lebanon ibaki kuwa nchi huru, inayojitegemea na yenye mamlaka kamili, na idumishe tofauti zake za kidini na kitamaduni, hususan mshikamano wa Kiislamu–Kikristo, ilhali baadhi ya mikondo ya kujitenga inafanya juhudi za kuzusha migawanyiko, uadui na kueneza chuki miongoni mwa makundi mbalimbali ya wananchi wa Lebanon.
Alivitaka baadhi ya vikundi vya kisiasa vinavyotegemea wageni na mabadiliko ya kikanda na kimataifa, kurejea upya mahesabu yao; kwani Lebanon, kwa kuendelea kwa mienendo ya makundi haya ambayo hayajafanya chochote zaidi ya kutoa misamaha bila kupata mafanikio ya kitaifa, kamwe haiwezi kuimarika wala kufanya kazi kwa ufanisi.
Sheikh Amrū alihitimisha kwa kusisitiza: Katika hatua hii ambayo kiwango cha mashinikizo ya kisiasa, kiuchumi, kimedia na kisaikolojia kimeongezeka, sote tumeitwa kusonga mbele kwa umoja na juhudi za pamoja ili kuilinda na kuihifadhi nchi yetu.
Maoni yako